Languages
25
Waimbaji

1 Daudi, pamoja na majemadari wa jeshi, wakawatenga baadhi ya wana wa Asafu, wana wa Hemani na wana wa Yeduthuni, kwa ajili ya huduma ya kutoa unabii, wakitumia vinubi, zeze na matoazi. Hii ndiyo orodha ya watu waliofanya huduma hii:

 
2 Kutoka kwa wana wa Asafu walikuwa:
Zakuri, Yosefu, Nethania na Asarela. Wana wa Asafu walikuwa chini ya usimamizi wa Asafu, ambaye alitoa unabii chini ya usimamizi wa mfalme.
3 Wana wa Yeduthuni walikuwa sita:
Gedalia, Seri, Yeshaya, Shimei, Hashabia, na Matithia, nao walikuwa chini ya usimamizi wa baba yao Yeduthuni, wao walikuwa wakitoa unabii wakitumia vinubi, wakimshukuru na kumtukuza Bwana.
4 Wana wa Hemani walikuwa:
Bukia, Matania, Uzieli, Shebueli na Yeremothi, Hanania, Hanani, Eliatha, Gidalti na Romamti-Ezeri, Yoshbekasha, Malothi, Hothiri na Mahaziothi. 5 Wote hawa walikuwa wana wa Hemani mwonaji wa mfalme. Aliwapata wana hawa kutokana na ahadi ya Mungu ili kumwinua. Mungu alimpa Hemani wana kumi na wanne na binti watatu.
 

6 Hawa wanaume wote walikuwa chini ya usimamizi wa baba yao kwa ajili ya uimbaji katika Hekalu la Bwana wakitumia matoazi, zeze na vinubi, kwa ajili ya huduma katika nyumba ya Mungu. Asafu, Yeduthuni na Hemani walikuwa chini ya usimamizi wa mfalme. 7 Pamoja na ndugu zao wote walikuwa wamefundishwa na kuwa stadi wa uimbaji kwa Bwana. Idadi yao walikuwa 288. 8 Vijana kwa wazee, walimu kwa wanafunzi, wote walipanga kazi zao kwa kupiga kura.