Zaburi 115
Mungu Mmoja Wa Kweli
1 Sio kwetu sisi, Ee Bwana , sio kwetu sisi,
bali utukufu ni kwa jina lako,
kwa sababu ya upendo
na uaminifu wako.
2 Kwa nini mataifa waseme,
“Yuko wapi Mungu wao?”
3 Mungu wetu yuko mbinguni,
naye hufanya lolote limpendezalo.
4 Lakini sanamu zao ni za fedha na dhahabu,
zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
5 Zina vinywa, lakini haziwezi kusema,
zina macho, lakini haziwezi kuona;
6 zina masikio, lakini haziwezi kusikia,
zina pua, lakini haziwezi kunusa;
7 zina mikono, lakini haziwezi kupapasa,
zina miguu, lakini haziwezi kutembea;
wala koo zao haziwezi kutoa sauti.
8 Wale wanaozitengeneza watafanana nazo,
vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia.
9 Ee nyumba ya Israeli, mtumainini Bwana ,
yeye ni msaada na ngao yao.
10 Ee nyumba ya Aroni, mtumainini Bwana ,
yeye ni msaada na ngao yao.
11 Ninyi mnaomcha, mtumainini Bwana ,
yeye ni msaada na ngao yao.
12 Bwana anatukumbuka na atatubariki:
ataibariki nyumba ya Israeli,
ataibariki nyumba ya Aroni,
13 atawabariki wale wanaomcha Bwana ,
wadogo kwa wakubwa.
14 Bwana na awawezeshe kuongezeka,
ninyi na watoto wenu.
15 Mbarikiwe na Bwana
Muumba wa mbingu na dunia.
16 Mbingu zilizo juu sana ni mali ya Bwana ,
lakini dunia amempa mwanadamu.
17 Sio wafu wanaomsifu Bwana ,
wale washukao mahali pa kimya,[~1~]
18 bali ni sisi tunaomtukuza Bwana ,
sasa na hata milele.
Msifuni Bwana .† Msifuni Bwana ni Kiebrania Hallelu Yah.
<- Zaburi 114Zaburi 116 ->
*Zaburi 115:17 Mahali pa kimya maana yake ni Kuzimu, yaani Sheol kwa Kiebrania.
†Zaburi 115:18 Msifuni Bwana ni Kiebrania Hallelu Yah.